Powered By Blogger

Monday 1 October 2012

Hatari ya Al-shaabab Nchini

Shambulio laua mtoto na kujeruhi wengine kanisani

Mtoto mmoja aliuawa papo hapo na wengine zaidi ya 10 wakajeruhiwa kwenye shambulio la guruneti katika Kanisa la St Polycarp ACK, barabara ya Juja, Mtaa wa Eastleigh, Nairobi, Jumapili.

Afisa mmoja wa matibabu katika hospitali ya Radiant, eneo la Mlango Kubwa, alisema mtoto huyo mvulana kwa jina Ian Mario Maina, aliyetimu umri wa miaka tisa Jumamosi, alipelekwa hospitalini akiwa tayari ameaga dunia.


“Alikuwa na majeraha mabaya mikononi, sehemu za tumbo na miguuni,” akasema afisa huyo, na kuomba tusimtaje jina kwa sababu hana ruhusa kuzungumza kwa niaba ya hospitali hiyo.

Biwi la simanzi lilitanda katika hospitali hiyo, huku marafiki wakimliwaza mama ya mtoto huyo, ambaye alilemewa na majonzi kwa kumpoteza mwanawe ghafla.

Watoto wanne waliokuwa na majeraha madogo miguuni na kichwani, na mwanamke aliyepatwa na mshtuko, walipelekwa Guru Nanak, huku saba waliojeruhiwa vibaya wakipelekwa katika hospitali ya Radiant iliyo karibu na kanisa hilo, kabla ya kuhamishwa hadi Kenyatta.

Mkuu wa Polisi eneo la Starehe, Bw Samuel Anampiu, wavamizi katika shambulio hilo lililotokea mwendo wa saa 4.30 asubuhi walitumia bomu la kujitengenezea.

“Maafisa wetu wamekusanya vipande ambavyo vitafanyiwa uchunguzi wa kina,” akasema.

Kujibizana

Iliripotiwa kuwa awali wanaume wawili walionekana wakijibizana na walinzi wa kanisa hilo kabla ya kuondoka kwa miguu.

Muumini mmoja wa kanisa hilo, Bi Anne Wanjiru Murage, alisema alisikia mlipuko kisha waumini wakaanza kutawanyika wakielekea mahali kunapokuwa na ibada ya watoto.

“Tuliskia mlipuko mkubwa kisha tukaona vumbi katika jengo ambamo watoto huwa na ibada yao,” akasema Bi Murage, ambaye alipeleka watoto wanne, akiwemo mwanawe, katika hospitali ya Guru Nanak.

Alisema bomu hilo lilitupwa kutoka nje ya kanisa, na kuanguka ndani ya darasa linalotumiwa kwa ibada ya watoto. “Kuna ua ambalo limezunguka kanisa na pia kuna askari wanaokagua kila mtu anayeingia kanisani. Bomu hilo lilirushwa kutoka upande wa nyuma, ambapo kanisa limepakana na maeneo ya makazi,” akasema.

Hali ya taharuki ilitanda katika eneo hilo baada ya wakazi wanaoaminika kuwa Wakristo kutishia kuwatimua wenzao wa Kiislamu.

Vijana hao waliojiunga kwa makundi walishambulia mijengo kadha kwa mawe na kutishia kuichoma moto.

Maafisa wa GSU waliungana na polisi wa kawaida katika kupiga doria mchana mzima ili kudumisha utulivu.

Mbunge wa Starehe, Bi Margaret Wanjiru, alitembelea eneo hilo na kukashifu kitendo hicho, huku akitaka Serikali ichunguze kwa kina kiini na wahusika wa shambulio hilo.

Washukiwa

Polisi walikamata watu wanne, ambao walijitambulisha kuwa wanahabari wa shirika la Horn Cable TV.

Kisa hicho kilitokea siku mbili tu baada ya wanajeshi wa KDF, wakishirikiana na wale wa Muungano wa Afrika (Amisom), kuwatimua wanamgambo wa Al-Shabaab kutoka ngome yao ya Kismayu, Somalia. Al-Shabaab wameapa kulipiza kisasi.

Kitengo cha habari cha Harakat Al-Shabaab Al Mujahideen, vuguvugu la utawala wa Kusini na Kati mwa Somalia, linaloshirikiana na Al-Shabaab, lilitangaza baadaye kuwa KDF ilidhihirisha vita vyao vilikuwa dhidi ya dini ya Kiislamu.

Kupitia mtandao wa 'Twitter’, utawala huo ulilaumu KDF kwa kuendeleza mashambulizi Kismayu licha ya kuwa wanamgambo walikuwa wameondoka.

Walidai kuwa watoto wawili walifariki katika mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia jana.



Maswala ya mashambulizi kutoka kwa kundi la Al-shabaabyanazidi kuongezeka huku Wanajeshi wetu wakipabana na kundi hili kule Somalia tukio hili linasemekana nikama majibu Kundi hili kwa Nchini hii baada ya KDF kuteka mji wa Kisimayu.

No comments:

Post a Comment